Jumatano , 3rd Aug , 2022

Wachezaji wa vilabu vya ligi kuu ya Uingereza wamekubaliana kusitisha rasmi ishara ya kupinga ubaguzi wa rangi kwa kupiga goti katika kila mchezo wa ligi hiyo kuanzia msimu mpya utakao anza ijumaa wiki hii.

Erling Haaland wa Manchester City na Trent Alexander-Arnold wa Liverpool wakiwa wamepiga goti kabla ya mchezo wa ngao ya jamii.

Manahodha wa vilabu hivyo wamefikia uamuzi huo baada ya kushauriana na wachezaji wenzao, na kusema ishara hiyo haina ulazima sana baada ya vitendo vya ubaguzi kupungua, na badala yake sasa ishara hiyo itafanyika katika kutoka hatua moja kwenda hatua nyingine kama vile hatua ya robo fainali, nusu fainali na fainali katika mashindano ya michezo mbalimbali.

Hivyo wachezaji na wafanyakazi wa viwanjani pia watapiga goti kabla ya mchezo wa kwanza wa ufunguzi wa ligi na michezo ya mwisho wa msimu 2022-23. Ishara hiyo ilifanyika kabla ya mchezo wa ngao ya jamii kati ya Liverpool na Manchester City Jumamosi iliyopita.

Vilabu vya ligi kuu ya Uingereza vilianza kupiga goti kuunga mkono vuguvugu la Black Lives Matter ambalo lilipata umaarufu kufuatia kifo cha George Floyd nchini Marekani mwezi Mei 2020.