Jumatano , 25th Feb , 2015

Makocha, waamuzi na wachezaji washiriki katika michuano ya wavu klabu bingwa mkoa wa Dar es salaam wametakiwa kufuata sheria za mchezo huo ili kuweza kuanza na kumaliza mchezo bila kuwa na malalamiko yoyote.

Akizungumza jijini Dar es salaam, Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Wavu Mkoa wa Dar es salaam DAREVA, Siraju Mwasha amesema, mashindano hayo yanayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Februari 28 mwaka huu Uwanja wa Shule ya Uhuru yanalengo la kukuza mchezo huo kwa vilabu mbalimbali hivyo vinatakiwa kuzingatia nidhamu ambayo ndiyo ngao ya michezo.

Mwasha amesema, vilabu hivyo vinatakiwa kuelewa ni mambo gani yanatakiwa ikiwa ni pamoja na kufuata sheria za mchezo huo pamoja na maelekezo yanayotolewa na makocha hao ili kuweza kushinda katika michuano hiyo.

Michuano hiyo itakuwa ikifanyika Jumamosi na Jumapili huku kukiwa na sehemu mbili ambapo ya kwanza itamalizika Aprili huku ya pili ambayo ni yakujua mshindi itamalizika Agosti mwaka huu.