Alhamisi , 28th Apr , 2016

Tanzania inataraji kupokea ugeni mkubwa wa wanamichezo wa mchezo wa riadha kutoka katika mataifa 11 ya ukanda wa Afrika Mashariki na Kati watakaotua nchini kushiriki mashindano ya riadha kwa vijana yatakayoanza kesho katika uwanja wa taifa.

Kikosi cha timu ya taifa ya riadha ya Tanzania.

Zaidi ya wanariadha vijana 150 kutoka mataifa 11 ya ukanda wa Afrika Mashariki na kati wanataraji kushiriki michuano mikubwa ya riadha kwa vijana wa chini ya miaka 20 kwa nchi za ukanda huo michuano itakayoanza kesho katika uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam nakumalizika siku ya jumamosi April 30.

Wanaridha hao wa michezo mbalimbali ya riadha kama mbio,kutupa mikuki, kutupa tufe na kuruka wanatoka katika nchi za Ethiopia, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Sudan, Djibout, Elitrea, Somalia, Zanzibar na wenyeji Tanzania bara ambayo itawakilsihwa na wanariadha zaidi ya 37.

Wakizungumzia maandalizi ya michuano hiyo viongozi wa chama cha riadha nchini RT, Wiliam Kalaghe ambaye ni makamu mwenyekiti, Omben Zavara ambaye ni kaimu katibu mkuu wamesema maandalizi yote yamekamilika na kimsingi timu ya taifa ya vijana ya Tanzania iko tayari kwa michuano hiyo hivyo ni vema kwa Watanzania wote hasa wakazi wa jijini Dar es Salaam wakajitokeza kuona vipaji vya wachezaji wao na kuwapa sapoti ya hali na mali ikiwemo kuwashangilia vijana hao ili wafanye vema katika michuano hiyo.

Naye mmoja wa waratibu wa riadha nchini ambaye kwa sasa anajishughulisha pia na masuala ya uchambuzi wa mchezo huo Wilhelm Gidabudai amesema mashindano hayo makubwa kwa vijana kufanyika nchini ni sifa ya kipekee na ni pongezi za dhati kwa chama cha riadha nchini RT na Serikali kwa ujumla kwa miundombinu mizuri ya uwanja wa taifa itakayotumika katika michuano hiyo ya siku mbili.

Gidabudai amesema mashindano hayo ambayo yanafanana kwa ukaribu na michuano ya kimataifa ya riadha ya Olimpiki itakuwa ni fursa kwa vijana na Wakitanzania kujitangaza kimataifa lakini pia kujiwekea rekodi na pia kufanya maandalizi ya kuwa kipimo chao kizuri kwaajili ya michuano ya Olimpiki ya Tokyo Japan.

Gidabudai ameongeza kusema kuwa mashindano hayo ni kipimo kizuri kwa wachezaji wazawa hasa kutokana na kushirikisha pia wanariadha wakali wenye uwezo na vipaji vya hali ya juu kutoka nchi kama Kenya na Ethiopia jambo ambalo litakuwa ni changamoto na kipimo kizuri kwao.