Hatua ya 16 bora ya Bball Kings kuanza kesho

Ijumaa , 6th Jul , 2018

Katika mwendelezo wa michuano ya Kikapu ya Sprite Bball Kings ambayo ilianza kwa mechi za mtoano wikiendi iliyopita sasa inaingia kwenye hatua ya 16 bora kwa jumla ya mechi 8 kupigwa wikiendi hii.

Moja ya mechi za hatua ya mchujo zilizofanyika Jumamosi iliyopita.

Michuano hiyo ambayo inadhaminiwa na kinywaji cha Sprite, itaendelea kesho Julai 7 kwenye viwanja vya Airwing Ukonga ambapo mechi 4 zitafanyika kwenye uwanja huo kuanzia saa 2:00 Asubuhi.

Mechi 4 zitakazopigwa uwanjani hapo ni kati ya Fast Heat dhidi ya DMI, Mbezi Beach KKKT dhidi ya Portland, Flying Dribblers dhidi ya Ukonga Hitmen na Ukonga Warriors dhidi ya Team Kiza.

Mechi za Jumapili zitakazopigwa kwenye uwanja wa Bandari Kurasini ambazo pia zitaanza saa 2:00 Asubuhi ni ile ya Raptors dhidi ya Water Institute, Ukonga Warriors dhidi ya Team Kiza na Stylers dhidi ya Temeke Heroes huku mabingwa watetezi Mchenga Bball Stars wakianza kutetea ubingwa wao dhidi ya Oysterbay.

Katika michezo hiyo ya kuwasaka wakali 8 watakaotinga hatua ya robo fainali haitakuwa na kiingilio hivyo mashabiki wa timu zote watapata nafasi ya kuhudhuria na kuzipa nguvu timu zao bila kulipa chochote. Pia timu nzima ya East Africa Television na East Africa Radio itakuwepo kutoa burudani mbalimbali ikiwemo mziki huku Sprite wao wakihusika na vinywaji.