Jumatano , 6th Apr , 2016

Klabu ya soka ya Azam fc hii leo imejikuta ikishindwa tena kwa mara ya pili mfululizo kula kiporo chake cha ligi kuu safari hii ikibanwa nyumbani na wamachinga kutoka Mtwara timu ya Ndanda fc wanakuchele katika uwanja wake wa nyumbani Azam Complex.

Kikosi cha timu ya soka ya Azam fc kikiwa katika uwanja wake wa nyumbani wa Azam Complex Chamazi.

Mabingwa wa soka wa klabu bingwa kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati [maarufu kombe la Kagaeme] ambao ni wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya kombe la shirikisho barani Afrika timu ya soka ya Azam FC hii leo wakiwa katika uwanja wao wa nyumbani Azam Complex Chamazi jijini Dar es Salaam wameshindwa kupunguza pengo la pointi mbele ya washindani wao wa ubingwa wa ligi kuu timu za Simba inayoongoza kwa alama 57 na Yanga yenye alama 53.

Sare ya mabao 2-2 dhidi ya wanakuchele Ndanda fc kutoka Mtwara imewaweka pabaya wanalambalamba hao ambao hivi majuzi walishindwa kupata alama tatu muhimu baada yakulazimishwa sare na wenyeji wao Toto Afrikacans ya Mwanza katika mchezo mkali uliochukua nafasi katika dimba la CCM Kirumba.

Sare hiyo dhidi ya Ndanda hii leo inamaanisha Azam fc sasa imeshindwa kula kiporo chake cha pili mfululizo kati ya viporo vitatu ilivyonavyo baada ya kukosa michezo kadhaa wakati ikiwa na majukumu ya kiamtaifa katika michuano ya CAF na hivyo matokeo hayo ni auheni ama nafuu kwa wapinzani wao Yanga ambao nao bado wanaviporo viwili kati ya vitatu walivyokuwa navyo huku pia nafuu ikiwa zaidi kwa vinara wa ligi hiyo timu ya Simba yenye alama 57 ambao walikuwa mbele kwa michezo mitatu zaidi na hivyo kuwa katika maombi ama dua la kuziombea timu za Azam na Yanga ziboronge michezo hiyo ya viporo ama viporo vyao vichache kitu ambacho kwa Azam kimeanza kujibu baada ya viporo viwili kuchacha kwa matokeo ya sare na hivyo timu hiyo kupoteza alama 4 kati ya sita.

Kwa matokeo hayo sasa msimamo wa ligi kuu Tanzania bara kwa sasa baada ya michezo miwili ya leo kwani kule mjini Songea mkoani Ruvuma wenyeji Majimaji ya huko imeendelea kuichimbia kaburi timu ya Wagosi wa kaya kutoka Tanga timu ya Coastal Union kwa kuididimiza kwa jumla ya mabao 2-0 katika mchezo mkali uliochukuwa nafasi katika dimba la Majimaji.

Matokeo kwa nafasi nne za juu ni kama ifuatavyo Simba ndio vinara wakiwa na alama 57 baada ya kucheza michezo 24, yanga wao wana alama 53 kwa michezo 22 huku Azam FC hii leo wakicheza mchezo wao wa 23 nakufikisha alama 52 na Mtibwa Sukari ambayo leo ilikuwa upambane na Yanga nayo iko katika mbio za ubingwa ikiwa na alama 42 kwa michezo 23.

Wakati huo huo timu ya soka ya Azam inaunganisha moja kwa moja katika kambi ya maandalizi ya mchezo wao wa kwanza wa nyumbani wakuwania kombe la shirikisho barani Afrika dhidi ya timu ngumu ya Esperance de Tunisie ya Tunisia katika mchezo utakaopigwa jumapili April 10 mwaka huu katika uwanja wa Azam Complex huko Chamazi nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa idara ya habari ya Azam fc kupitia kwa msemaji wa timu hiyo Jafar Idd Maganga amesema maandalizi ya mchezo huo yamekamilika na wapinzani wao timu ya Esperance watawasili April 8 mwaka asubuhi huku pia waamuzi wa mchezo huo kutoka Afrika kusini na Zambia nao wakitua nchini usiku wa siku hiyo hiyo.