Jumamosi , 14th Mei , 2016

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe, ametamka wazi kuwa wachezaji wote wanaoweka fedha mbele na wasiokuwa na mapenzi na timu hiyo hawatakuwa nao msimu ujao kwakuwa ndiyo wamechangia timu hiyo kukosa ubingwa wa msimu huu.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe.

Hans Poppe ameyasema hayo baada ya hivi karibuni baadhi ya wachezaji wa Simba kugoma kwenda Songea kucheza mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Majimaji wakishinikiza kulipwa mishahara yao.

Wachezaji waliogoma ni wale wa kigeni ambao ni Hamisi Kiiza, Juuko Murshid, Emery Nimubona, Justice Majabvi, Vincent Angban, Brian Majwega na Paul Kiongera, lakini baadaye Majabvi na Angban waliungana na timu japo Angban akucheza kabisa huku Majabvi yeye akiingia kipindi cha pili.

Hans Poppe amesema: “Hatutaendelea kuwa na wachezaji wasiokuwa na mapenzi na timu, haiwezekani mshahara uchelewe kidogo halafu unagoma, mbona hata serikalini mishahara inachelewa na watu wanafanya kazi kama kawaida huku wakifuatilia haki yao kwa utaratibu lakini kwa wachezaji wa Simba imekuwa tofauti wamekuwa wakicheza ilimradi nakupelekea matokeo mabovu kwa timu hiyo na sasa imepoteza tena nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa kwa msimu wa nne.

Poppe ambaye kwa sasa ndiyo kama mhimili wa timu hiyo amesema “Hii haipo Simba tu, wanapaswa kutambua kwamba wapo kwa ajili ya kuipigania timu na masuala hayo yakitokea si sisi bali mazingira ndiyo husababisha, bora tubaki na wachezaji wenye mapenzi na timu kuliko wa aina hii awana uchungu na timu.”

"Hebu angalia sasa wamelipwa na walicheza kinazi na timu imepoteza nafasi ya ubingwa na uwakilishi wa michuano ya Kimataifa sasa hiyo mishahara wameifanyika kazi gani wakati wameharibu," alihoji Hans Poppe.

Kauli hiyo ya Hans Poppe inamaanisha kuwa, Kiiza na Juuko wana nafasi ndogo ya kubaki Simba kwani huwa hawataki kucheleweshewa mishahara yao.

Kiiza amekuwa akilaumiwa kwamba amekuwa chanzo cha migogoro ya chini chini ndani ya klabu hiyo hali inayosababisha mfarakano kati ya wachezaji na viongozi na kupelekea timu hiyo ambayo ilikuwa katika mbio za ubingwa kupoteza mwelekeo dakika za mwisho na kutoa mwanya wa mahasimu wao Yanga kuendelea kutamba.

Hivi karibuni, Kiiza aliwahi kufukuzwa kambini kutokana na utovu wa nidhamu na uamuzi huo ulichukuliwa na meneja wa Simba.

Simba sasa baada yakupoteza mwelekeo kutokana na kukosa mshikamano baina ya wachezaji, benchi la ufundi, viongozi na wanachama wamekuwa katika malumbano ya chini chini baina yao huku mashabiki na wanachama wakipiga kelele na kupaza sauti zao kuutaka uongozi wao ujiuzuru ama uitishe mkutano mkuu wa dharula kujadili mustakabali wa timu hiyo.