Jumamosi , 16th Jun , 2018

Timu ya mpira wa Kikapu ya TMT ambayo ilishika nafasi ya pili msimu uliopita nyumba ya mabingwa Mchenga Bball Stars, imeeleza hofu yake kwenye hatua ya mchujo kutokana na hali halisi ya maandalizi ya timu zilizojisajili.

Akiongea leo kwenye usaili wa timu unaofanyika Mlimani City nahodha wa TMT Is-haka Masoud amesema ameona timu nyingi anazozifahamu zimejiandikisha hivyo anaamini kuvuka hatua ya mchujo haitakuwa rahisi kwao.

''Naweza kusema mwaka huu timu zimejiandaa unajua sisi tunafahamiana kwahiyo kuna timu zimesajili hapa nazijua na ni bora sana lakini sisi tutajitahidi kuhakikisha tunavuka kwenye hatua ya mchujo ili twende mbele zaidi'', amesema.

Maosud amesema pamoja na changamoto hizo lakini mipango yao mwaka huu ni kuchukua ubingwa huku wakiwa na hamu ya kulipa kisasi kwa wanafainali wenzao Mchenga Bball Stars.

Aidha nahodha huyo amesema mashindano ya Sprite Bball Kings msimu ulipopita yamesaidi vipaji vingi kuonekana na timu za ligi kuu RBA na kupaat usajili hivyo anaamini msimu huu vijana wengi wataonesha vipaji zaidi.

Masoud ameweka wazi kuwa TMT imefanya usajili wa wachezaji wapya watatu huku wengine saba wakiwa ni walewale walioshiriki msimu uliopita lakini wamejifua vyema kuhakikisha wanachukua Kombe na milioni 10 za bingwa.