Jumatatu , 20th Jan , 2020

Ni takribani siku ya tano sasa tangu zilipoibuka tetesi juu ya mshambuliaji wa Genk na timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars', Mbwana Samatta kuwaniwa na klabu ya Aston Villa.

Mbwana Samatta

Watanzania wanasubiri kwa hamu kubwa kusikia taarifa ya utambulisho wa Samatta hasa katika mitandao yake ya kijamii, ambako Watanzania wamezidi kuifuatilia. Hilo linajidhihirisha hata katika 'comments' zilizopo katika kurasa za Twitter na Instagram za klabu hiyo.

Taarifa hizo ziliripotiwa na mitandao yote mikubwa nchini Uingereza na Ubelgiji, Januari 17 kuwa Aston Villa imemmulika Samatta kuwa ni mbadala katika safu ya ushambuliaji baada ya kuumia kwa mshambuliaji wao tegemeo, Wesley Moraes, ambapo dau lililotajwa kwenye uhamisho huo ni Pauni milioni 8.5.

Siku iliyofuata Januari 18 ziliripotiwa taarifa kuwa Genk imeshamalizana na Aston Villa na Samatta ametua Jijini Birmingham nchini Uingereza kwa ajili ya vipimo vya afya na kukamilisha dili hilo.

Kinachoendelea hivi sasa ni kwamba Samatta amekamilisha vipimo vya afya na klabu hiyo na kinachosubiriwa ni ukamilishwaji wa masuala machache ikiwemo vibali vya kazi. Januari 18, mtangazaji maarufu wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC, Salim Kikeke alithibitisha kuwa kila kitu kimekwenda sawa na kinachosubiriwa ni utambulisho wake.

Aston Villa itawakaribisha Watford katika uwanja wake wa nyumbani, kesho Jumanne katika mchezo wa ligi kuu nchini Uingereza. Kuna uwezekano mkubwa wa kukosekana kwa Samatta kwenye mchezo huo, kwani mpaka sasa hajatambulishwa rasmi.