Jumatatu , 30th Mar , 2015

Timu ya Yanga inatarajia kuelekea Bulawayo Nchini Zimbabwe Jumatano ya wiki hii kwa ajili ya maandalizi ya mechi ya marudiano dhidi ya Timu ya FC Platinum itakayochezwa kati ya Aprili 3, 4 au 5 mwaka huu.

Akizungumza na East Africa Radio, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga, Jerry Muro, amesema wachezaji wa Timu hiyo waliokuwa kambini katika Timu ya Taifa Stars wamewasili leo na wameshaanza mazoezi ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mechi hiyo.

Muro amesema, wanaamini watafanya vizuri kutokana na mfumo wa mazoezi na kadri siku zinavyozidi kusonga mbele ndivyo mazoezi yanaimarika na kila kitu kimekamilika kwa ajili ya safari hiyo na wana uhakika wa kufanya vyema na kuwang'oa wapinzani wao hao.

Yanga SC ilitanguliza mguu mmoja kusonga katika hatua ya pili ya michuano hiyo baada ya kuibuka na ushindi mnono wa mabao 5-1 dhidi ya timu ya FC Platinum iliyoing'oa Sofapaka FC ya Kenya katika hatua ya awali.

Endapo Yanga SC ikifanikiwa kuwang'oa Wazimbabwe hao, itakutana na mshindi kati ya Benfica FC ya Angola na Etoile du Sahel ya Tunisia katika hatua inayofuata ya michuano hiyo ya pili kwa ukubwa barani Afrika katika ngazi ya klabu.

Benfica FC na Etoile du Sahel FC iliyomnunua Emmanuel Okwi wa Simba SC misimu miwili iliyopita, ni miongoni mwa timu tajiri barani Afrika na zimekuwa zikisajiri wachezaji 'mafundi' na wenye uwezo mkubwa.

Etoile du Sahel FC ilishinda 1-0 katika mechi ya kwanza iliyochezwa mjini Tunis, Tunisia wiki mbili zilizopita.