Jumamosi , 7th Mei , 2016

Wawakilishi pekee wa Tanzania katika michuano ya Afrika, Yanga SC leo inashuka dimbani uwanja wa Taifa, Dar es Salaam dhidi ya Sagrada Esperanca ya Angola.

Huu ni mchezo wa kwanza wa mchujo wa kuwania kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika na timu hizo zitarudiana wiki ijayo Angola.

Katika mchezo wa leo Yanga itawakosa wachezaji wake wawili tegemeo wa kimataifa wa Zimbabwe, kiungo Thabani Scara Kamusoko na mshambuliaji Donaldo Dombo Ngoma, ambao wanatumikia adhabu ya kadi za njano mfululizo walizopewa katika mechi dhidi ya Al Ahly mwezi uliopita.

Mchezo huo utachezeshwa na marefa kutoka Ghana, ambao ni Joseph Odartei Lamptey atakayepuliza filimbi akisaidiwa na washika vibendera David Laryea na Malik Alidu Salifu, wakati Kamisaa ni Asfaw Luleseged Begashaw kutoka Ethiopia.

Mchezo wa marudiano utachezeshwa na marefa wa Madagascar Mei 17 mwaka huu uwanja wa Sagrada Esperanca, zamani Quintalao do Dundo.

Yanga imeangukia katika kapu la kuwania kucheza hatua ya makundi ya shirikisho, baada ya kutolewa na Al Ahly ya Misri katika hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 3-2, ikilazimishwa sare ya 1-1 Dar es Salaam na kufungwa 2-1 Alexandria.