Yanga SC kuwakosa nyota wake 3 kesho

Jumanne , 13th Feb , 2018

Timu ya Mabingwa wa soka Tanzania Bara Yanga SC inatarajiwa kushuka dimba la Uhuru Jijini Dar es Salaam kesho kuvaana na Majimaji FC huku ikiwakosa nyota wake watatu ambao bado ni majeruhi mpaka sasa.

Hayo yamebainishwa na taarifa zilizotolewa na uongozi wa timu hiyo kupitia moja ya kurasa zao za mitandao ya kijamii ambapo wamedai maandalizi dhidi ya mchezo huo wa muendelezo wa VPL dhidi ya Majimaji FC yamekamilika mpaka sasa.

"Tuko tayari kwa mchezo wa kesho, lakini hatutakuwa na wachezaji watatu ambao ni Yohana Mkomola, Amisi Tambwe pamoja na Donald Ngoma kutokana bado ni majeruhi hivyo hawatakuwa sehemu ya mchezo", imesema taarifa hiyo.

Kwa upande mwingine, timu ya Yanga imethibitisha kuwa ipo tayari kwa ajili ya safari yake kuelekea Shelisheli kwenye mechi ya marudiano dhidi ya St. Louis ambapo timu hiyo inatarajiwa kuondoka nchini Jumapili.