Ijumaa , 22nd Jan , 2016

Kocha msaidizi wa timu ya Yanga Juma Mwambusi amesema, wanaangalia uwezo wa kiungo wa klabu hiyo Haruna Niyonzima ambaye ameanza mazoezi leo kama ataweza kuanza katika mchezo wa kwanza katika michuano ya Kombe la Shirikisho FA Cup.

Mwambusi amesema, kama yupo vizuri ataanza na mchezo wa kwanza na kama hatokuwa vizuri bado kuna mechi nyingine nyingi ambazo ataweza kucheza kwani amerejea kwenye kikosi na amepokelewa vizuri kwa kuwa ni mchezaji wa kikosi hicho.

Mwambusi amesema, kesho wanafanya mazoezi ya mwisho kwa ajili ya kuvaana na Friends Rangers katika mzunguko wa tatu wa FA hivyo wataweza kuendelea kuangalia na kupima uwezo wake.

Kwa upande wake Haruna Niyonzima amesema, chochote kinaweza kutokea kutokana na uwezo atakaouonesha katika mazoezi lakini anajiamini anaweza na atafanya vizuri katika kikosi chake.

Niyonzima amesema, anajiamini yeye ni mzuri lakini hakuna mchezaji mmoja mzuri kwa sababu timu ni kama familia na hawezi kucheza peke yake bila ushirikiano na wachezaji wenzake na kwa sasa anaangalia mbele zaidi ili kuweza kufanya mazuri zaidi katika klabu yake japo haujui mpira lakini anaijua kazi yake.