Jumapili , 7th Feb , 2016

Unaweza kusema kwamba safari ya ubingwa wa ligi kuu ndio kama inaanza hasa kufuatia mbio za kufukuzana baina ya vigogo wa ligi hiyo Yanga, Simba na Azam hasa kutokana na timu hizo kupishana kwa utofauti mdogo wa alama moja katika msimamo wa ligi kuu.

Mabingwa watetezi wa ligi kuu ya soka Tanzania bara.

Ushindani wa ligi kuu ya soka Tanzania bara umeendelea kuwa mzito mara baada ya hii leo vigogo wa ligi hiyo wote kupata matokeo ya ushindi katika michezo yao na hivyo kuongeza ushindani katika mbio za kuwania ubingwa wa ligi kuu Tanzania Bara.

Safari hii mshindi ni mmoja tu yaani bingwa pekee ndiye atapata tiketi ya uwakilishi wa nchi katika michuano ya vilabu barani Afrika huku nafasi ya pili ikienda kwa atakayetwaa ubingwa wa kombe la shirikisho ambalo nalo pia vigogo hao wamo na wametinga hatua ya 16 bora.

Katika ligi kuu hii leo mabingwa watetezi wa ligi hiyo wanajangwani Yanga wamerejea kwa kishindo na kufuta makosa yao ya kuboronga michezo yao miwili iliyopita mara baada ya kuwasulubu maafande wa JKT Ruvu kwa jumla ya mabao 4-0 katika mchezo uliochukua nafasi katika dimba la taifa jijini Dar es Salaam.

Magoli ya Yanga katika mchezo wa leo ambao JKT Ruvu ndiyo walikuwa wenyeji yalifungwa na Simon Msuva aliyepachika mabao mawili, mzimbabwe Donald Ngoma pamoja na Mniger Isoufou Boubacar na kuifanya timu hiyo kujikita kileleni mwa ligi hiyo kwa alama 43 baada yakushuka dimbani mara 18 .

Na huko katika uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga bao pekee la mshambuliaji Ibrahim Hajib limeipa Simba SC ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wenyeji Kagera Sugar.

Ushindi huo unaifanya Simba SC iendelee kukaa nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu, ikifikisha pointi 42 baada ya kucheza mechi 18.

Hajib alifunga bao hilo dakika ya 45 baada ya kupata pasi ya kisigino ya Mganda, Hamisi Kiiza baada ya awali kiungo fundi wa timu hiyo Mwinyi Kazimoto kufanya kazi nzuri ya upishi wa bao hilo.

Nao mabingwa wa kombe la klabu bingwa kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati Azam FC wamerejea kwa kishindo katika ligi hiyo baada ya kuutumia vema uwanja wake wa nyumbani kufuatia ushindi wao wa bao 1-0 dhidi ya wachimba migodi toka Shinyanga timu ya Mwadui FC, shukrani pekee kwa goli la mshambuliaji raia wa Ivory Coast Kipre Tchetche, ushindi ambao unaifanya timu hiyo kufikisha alama 42 lakini ikiwa nyuma michezo miwili.