Wachezaji wa Tanzania Mbwana Samata na Tomas Ulimwengu wanataraji kuja nchini na timu yao ya TP Mazembe ya Congo DR.
Timu hiyo yenye Watanzania wawili, Mbwana Ally Samatta na Thomas Emmanuel Ulimwengu itakuwa na mchezo mgumu wa ugenini dhidi ya Al Hilal nchini Sudan Jumapili ya Agosti 23, mwaka huu na kuelekea mechi hiyo itakuja kuweka kambi Dar es Salaam.
Taarifa za kutoka ndani ya uongozi wa Azam fc zinasema timu ya TP Mazembe wameomba kutumia Uwanja wa Azam FC kwa mazoezi ya kujiandaa na mechi za ligi ya mabingwa barani Afrika.
Uongozi huo umesema ''Mazembe wanataka kuja kutumia vifaa vyetu kwa maandalizi kwa maana ya Uwanja wa mazoezi na vitu vingine ikiwemo gym. Kimsingi tumewakubalia na kuna uwezekano pia tukacheza nao mchezo wa kirafiki,''.
Kikosi cha Azam FC kipo kambini visiwani Zanzibar kujiandaa na mchezo wa Ngao ya Jamii Agosti 22 dhidi ya mabingwa wa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara, Yanga SC na kinaweza kurejea Dar es Salaam kucheza na Mazembe.
Haijajulikana kama Mazembe itakuwa tayari kucheza mechi zaidi za kujipima nguvu na vigogo wa hapa nchini yaani Simba na Yanga ambao nao wangependa changamoto hiyo kutoka kwa matajili hao wa Congo DR.
Ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Smouha ya Misri mjini Lubumbashi umeipandisha kileleni mwa Kundi A Mazembe katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
Katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Mazembe, bao pekee la TP Mazembe lilifungwa na Roger Assale dakika ya 53 na sasa mabingwa hao mara nne Afrika wanatimiza pointi nane baada ya kushinda mechi mbili na sare mbili.
Al Hilal inabaki na pointi zake tano baada ya juzi kufungwa 1-0 nyumbani na Moghreb Tetouan ya Morocco ambayo sasa nayo imefikisha pointi tano. Smouha ya Misri ina pointi tatu.