Mmoja wa wanachama wa Simba SC ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tawi la Mpira Pesa Ustadh Masoud amesema, mchezo huo wanautazama kwa hali ya kawaida sana kwani wameshakutana na Yanga mara nyingi na wote wanapatikana sehemu moja lakini wanaamini wataibuka na pointi tatu katika mchezo huo.
Ustadh amesema, hawawezi kuzungumzia magoli kwa sababu walishawafunga Yanga magoli mpaka sita hivyo kuzungumzia suala hilo halitakuwa na maana labda Yanga ndio watakuwa na idadi ya magoli kwani wao wanachokitafuta zaidi ni pointi tatu.
Ustaadh amesema, muamuzi anatakiwa kuchezesha mchezo kwa usawa na haki kwa kufuata sheria zote 17 za soka na kama ana ushabiki na timu anatakiwa kuuweka pembeni na kuwaacha wachezaji wa Simba na Yanga wacheze mpira
Ustaadh amesema siku zote wapinzani wao hawajui kucheza mpira ndio maana muda wote Yanga wanakuwa na wasiwasi katika michezo yote wanayokutana.
Kwa upande wake mwanachama wa Klabu ya Yanga Khamisi Matandula amesema ana asilimia 90 za kushinda mchezo wa Jumamosi dhidi ya watani wao Simba japo watani wao pia wamejipanga na wana timu nzuri lakini mpira wa Simba na Yanga hautabiriki ingawa anaimani ya kuibuka na ushindi.
Matandula amesema, pengo la mshambuliaji Kelvin Yondani limeshazibwa ili kuweza kupata ushindi na mashabiki wenye imani ndogo watazimia sana katika mchezo huo pamoja na wengine kupigana kama wasipokuwa na uvumilivu katika mchezo huo.
Matandula amesema, katika mchezo wa watani wa jadi Simba na Yanga shabiki anatakiwa kujiandaa kwa matokeo matatu ya kufunga kufungwa na hata sare kwani baada ya dakika 90 wote ni ndugu.
Matandula amesema, waamuzi ndio mara zote wanakuwa na matatizo na ndio maana mchezo unapomalizika wanakimbilia sehemu yenye usalama kwa sababu wanajua walichokifanya uwanjani.
Huu ni mchezo wa marudiano ambapo katika mchezo wa awali iliyopigwa Septemba 26 Mwaka jana Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, Yanga iliweza kuilaza Simba SC bao 2-0 mabao yaliyofunga na Amisi Tambwe na Malimi Busungu.