Jumatano , 11th Mei , 2016

Waziri wa Tamisemi Mhe. George Simbachawene ameombwa kuingilia kati zoezi la kuwatoa wafanyabiashara wadogowadogo maarufu kama machinga baada ya uongozi wa mkoa kutajwa kushindwa kutatua suala hilo ambalo aliwezi kuleta matokeo chanya endapo nguvu

zitatumika.

Akiongea na East Africa Radio Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wenye Viwanda na Biashara Ndogodongo (VIBINDO) Bw. Gaston Gikuyi amesema, tangu mwezi wa tatu wamefanya jitihada nyingi za kuonana na mkuu wa mkoa hata kujaribu kwanjia ya mawasiliano bila mafanikio na badala yake manyanyaso kwa wamachinga yanachukuliwa kama ndio suluhisho bila kuwashirikisha viongozi wao.

Bw. Gaston amesema jumuiya yao imekuwa ikitoa mapendekezo kadhaa ya jinsi serikali inavyoweza kutatua uwepo wa machinga maeneo ya miji yote nchini lakini viongozi wameshindwa kuthaamini michango yao suala ambalo linazidi kuchelewesha jitihada ya kuwa na maeneo mahususi kwa ajili yao.

"Unatenga eneo nje ya mji kwa ajili ya Machinga, ambako hakuna biashara alafu unataka watii sheria ni heri kuvunja sheria ili uishi kuliko kufuata sheria ili ufe, kutatua jambo hili kunahitaji utashi mkubwa sio nguvu kwa kuwatesa machinga," amesema Bw. Gaston.

Aidha, Bw. Gaston amewataka viongozi wa serikali kuacha tabia ya kutoa majibu mepesi kwenye maswali magumu jambo ambalo linaendeleza migogoro kati ya serikali na wafanyabiashara wadogo wadogo, na kuongeza kuwa viongozi pia wanajisahau kuwa wamachinga wanachangia kuendeleza uchumi wa nchi na kutatua tatizo la ukosefu wa ajira ambao serikali imeshindwa kutekeleza kikamilifu.

“Serikali imeshindwa kuajiri watu, wanajiajiri bado awatengenezi mazingira rafiki kwa shuguli zao, hivi juzi tuu waliahidi kuwasaidia machinga na kura zao wakawapa lakini sasa hivi wamesahau na kuanza kuwafukuza, ” alisema Bw. Gaston

Bw. Gikuyi amesema katika jiji la Dar es Salaam kuna wamachinga zaidi ya laki 7 ambao nao wanafamilia zinazoishi kwa kuwategemea, kuwaondoa eneo ambalo linabiashara na kuwapeleka nje ya mji nikuua mitaji yao na kuzinyima familia za watu zaidi ya milioni mbili mahitaji muhimu.

Baadhi ya machinga waliopata fursa ya kuongea na East Africa Radio katika soko la Kariakoo wamesema serikali iwapatie eneo kwenye mikusanyiko ya watu ili wamudu kufanya biashara zao na sio kuwapatia maneo ya nje ya mji ambayo hayana tija kulingana na mitaji na aina ya biashara zao kwani wengi wanabiashara za mikononi hivyo kuwa mbali na mji nikuwanyima fursa ya kujipatia kipato.