Ijumaa , 20th Mei , 2016

Watu wasiojulikana wamemuua kwa kumpiga risasi kadhaa askari wa Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Ally Kinyogoli, jana majira ya saa moja usiku wakati akiwa nyumbani kwake Mkoani Pwani.

Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga.

Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema watu hao wawili wakiwa na Pikipiki aina ya Boxer, walifika nyumbani kwa askari huyo maeneo ya Mwandege Wilayani Mkuranga mkoani Pwani.

Kamanda Mpinga amesema baada ya kufika nyumbani kwa askari Kinyogoli, alitoka ili kuwasikiliza ndipo watu hao wakaanza kumshambulia kwa risasi na moja ya risasi hizo ikampata tumboni, na kufariki dunia wakati akikimbizwa hospitali.

Kamanda Mpinga amesema kuwa Jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi ili kuwabaini watuhumiwa hao ili sheria ichukue mkondo wake huku akionyeshwa kusikitisha juu ya tukio hilo lilitokea mbele ya mtoto wa marehemu.

Aidha, Kamanda Mpinga amesema marehemu atazikwa leo saa kumi nyumbani kwao kitunda maeneo ya Ukonga Jijini Dar es Salaam.