Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imesema ziara ya kikazi ya siku 5 nchini China iliyofanywa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje Dkt. Aziz Mlima imeleta mafanikio makubwa nchini hasa katika nyanja za siasa, uchumi na utamaduni.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya serikali kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bi. Mindi Kasiga amesema akiwa nchini China Dkt. Mlima pamoja na mambo mengine alipata fursa yakufanya mazungumzo makampuni makubwa yaliyoonyesha yanadhamira ya dhati yakuwekeza nchini hasa kwenye masuala ya uchumi kupitia uwekezaji kwa sekta ya Viwanda, Nishati na Miundombinu.
Amesema China imeweka kipaumbele cha juu katika miradi ya ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo, eneo la viwanda pamoja na maboresho ya Reli ya TAZARA na ipo tayari kuanza upembuzi yakinifu kwa maboresho ya Reli ya Kati.
Kuhusiana na awamu ya kwanza ya mkutano wa mazungumzo ya usuluhishi wa mgogoro wa Burundi ambao ulianza wiki iliyopita mkoani Arusha ambao unaoongozwa na Rais Mstaafu wa Tanzania Mhe. Benjamin William Mkapa amesema bado wanafanya majumuisho yake na watatoa tamko rasmi kwa vyombo vyote vya habari nchini ili Wanajumui ya Afrika Mashariki wajue kinachoendelea ndani ya Jumuiya hiyo.