Alhamisi , 3rd Nov , 2016

Watu watano wanashikiliwa na polisi mkoani Mtwara kwa tuhuma za kukutwa na vipodozi feki.

Vipodozi

 

Watu hao wameshikiliwa mara baada ya msako uliofanywa na Mamlaka ya Chakula na Dawa Mkoani humo kwa kushirikiana na jeshi la polisi kwa ajili ya kudhibiti uuzwaji huo wa vipodozi wenye madhara kwa binadamu.

Vipodozi hivyo ambavyo vingine muda wake wa matumizi umekwisha na vina viambata vyenye sumu vimekamatwa katika maduka mbalimbali kwenye manispaa ya Mtwara mikindani vikiwa na thamani ya zaidi ya shilingi milioni nane.

Akizungumza na waandishi wa habari afisa kutoka Mamlaka ya Dawa na Chakula Mkoani humo Bw. Mhagama amesema kuwa lengo la kufanya msako huo ni kuhakikisha kuwa bidhaa hizo hazitumiki kabisa katika manispaa hiyo na hatua kali zitashukuliwa kwa yeyote atakayekutwa ameviingiza au kuuza wilayani humo.

Kwa upande wa Kamanda ya Polisi Mkoa wa Mtwara, Thobias Sedoyeka amethibitisha kukamatwa kwa watu hao na kusema kuwa jeshi hilo litaendelea kuwasaka wale wote wanaofanya biashara hiyo kinyume cha sheria.