Jumapili , 5th Feb , 2017

Bao la Yahya Mohamed raia wa Ghana dakika ya 86 limetosha kuipa Azam Fc ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ndanda FC katika mchezo wa ligi kuu Tanzania Bara uliopigwa usiku huu katika dimba la Azam Complex Chamazi.

Wachezaji wa Azam FC wakishangilia bao

Azam wamepambana licha ya kukutana ushindani mkali, huku ikishindwa kutumia nafasi za wazi ilizotengeza ikiwemo ya dakika ya 51 ambapo Shaaban alikosa bao la wazi baada ya kupiga mpira uliotoka pembeni ya lango akiwa na kipa wa Ndanda kufuatia pasi safi aliyopigiwa na Yahaya

Hadi mwisho wa mchezo Azam imejivunia point zake 3 na kuendeleza rekodi ya kutofungwa katika mechi 10 mfululizo za mashindano, pia tangu kuanza kwa mwaka huu ikiwa haijapoteza mchezo wowote, na golikipa wake Aishi Manula akiwa amefungwa bao moja pekee.

Ushindi huu pia ni kulipa kisasi kwa Ndanda ambayo iliifunga Azam FC katika mchezo wa raundi ya kwanza mabao 2-01

Mara baada ya mchezo Nahodha wa Ndanda FC Ibrahim Hassan anasema matokeo hayo yanawaumiza kwa kuwa haikuwa malengo, lakini wamepambana kwa kadri ya uwezo wao licha ya bahati kutokuwa upande wao.

Kwa upande wa Azam FC, Himid Mao amesema kwa kuwa wamedhamiria kupata pointi 3 kila mchezo, hivyo kwa mchezo wale licha ya ukweli kuwa ulikuwa ni mchezo mgumu lakini wachezaji wenzake wamepambana kwa uwezo wao wote na kuhakikisha lengo la point 3 linatimia.

Azam sasa inafikisha point 37 katika nafasi ya tatu sawa na Kagera Sugar, lakini ikiizidi kwa uwiano wa magoli.

Katika mechi nyingine iliyopigwa leo, Mbeya City ikiwa nyumbani imeichapa JK Ruvu bao 1-0 likifungwa na Tito Okello katika dakika ya 40.