
Mwenyekiti wa CHADEMA taifa, Freeman Mbowe akiwa na Mbunge wa Tarime mjini Ester Matiko.
Jaji Rumanyika amefanya uamuzi huo baada ya Wakili wa Mbowe na Matiko, Wakili Peter Kibatala kudai kuwa nyaraka za uamuzi wa kesi ya warufani hao kutokea Mahakama ya Kisutu hazionekani.
Baada ya kueleza hayo Jaji Rumanyika aliomba apewe namba za Karani wa Kisutu ili aweze kumpigia simu akiwa ndani ya chumba cha mahakama.
Jaji Rumanyika alimpigia simu Karani huyo na kuweka Loud Speaker, ambapo alijitambulisha kuwa yeye anaitwa Rumanyika yupo Mahakama Kuu na anaulizia kwanini nyaraka za uamuzi wa mwenendo wa kesi ya Mbowe na wenzake hazijakamilika.
Karani huyo alijibu kuwa ni kweli anaifahamu kesi hiyo na nyaraka nyingine zinaendelea kuchapwa, hivyo hazijakamilika.
Jaji Rumanyika alimtaka Karani huyo kuhakikisha hadi ifikapo saa 7 mchana wa leo awe ameziwasilisha nyaraka hizo hata kama hazijachapwa ili ziweze kupitiwa na pande zote baina ya Warufani na Upande wa Mashtaka.
Awali wakili wa mashtaka, Faraja Nchimbi, aliiomba Mahakama iahirishe kesi hiyo hadi Ijumaa ili wapate muda wa kupitia nyaraka hizo, ambapo Wakili Kibatala alipinga na kutaka iahirishwe hadi saa 10 jioni ya leo.
Baada ya mvutano huo wa pande mbili, Jaji Rumanyika alichukua uamuzi wa kuhairisha kesi hiyo hadi kesho saa 2 asubuhi.
Katika kesi ya msingi iliyopo Mahakama ya Kisutu, Mbowe na wenzake wanakabiliwa na mashtaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai kati ya Februari 1 na 16, 2018, Dar es salaam