Jumanne , 13th Oct , 2020

Aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa ufundi wa Shirikisho la mpira wa miguu nchini TFF, Sunday Kayuni amesema ataendelea kulia na Serikali kwa kutorejesha mitaala ya michezo mashuleni jambo analoamini ninakwamisha maendeleo ya michezo.

Aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa ufundi wa TFF, Sunday Kayuni akikabidhi cheti kwa mmoja wa wanafunzi wa kozi za mpira nchini.

Kayuni ameyasema hayo kufuatia wadau wa michezo nchini kulitupia lawama Shirikisho la mpira wa miguu na Vilabu, kwa madai kwamba ndio chanzo cha timu ya Taifa ya Tanzania kufanya vibaya.

''Mpira nimali ya vilabu,TFF inatoa muongozo tu, na vilabu ndivyo vinavyotengeneza wachezaji ambao wanalitumikia taifa, lakini hawa wote wanaitegemea Serikali na hivyo vilabu vinategemea wachezaji kutoka mashuleni.

''Binafsi sitoacha kuipigia kelele Serikali na nitailaumu kwa kuwa hadi leo haijaridhia kurejesha michezo mashuleni, na kama Serikali haijaridhia michezo irejeshwe mashuleni hakuna sehemu tutakayofika'', amesema Kayuni.

Kayuni ameongeza kuwa, ''Tanzania ni nchi pekee duniani nadiriki kusema imeamua kuifanya michezo sio sehemu ya mtaala wa masomo mashuleni, huwezi kuweka kipindi cha dakika 90 siku ya Ijumaa pekee ukadhania utapeleka somo kwa wachezaji''.

Kayuni ameendelea kueleza kuwa, umri wa kuwafundisha watoto ili waelewe masomo ya michezo, yakiwemo nidhamu na namna ya kujitunza ikiwemo misingi yote ni muda wanaokuwa shuleni, hivyo leo hii kina Jonas Mkude watalaumiwa bure na makocha watatimuliwa lakini si kosa lao.

Kwa upande wa wachezaji amesema kwasasa hivi tunawachezaji wadhaifu, hawawezi kupambana na wenzetu, ndio maana Simba, Yanga, Azam wamejaa wachezaji wakigeni, na hizo timu zinamahitaji makubwa na zinasajili wageni kwakuwa waliopo Tanzania wanakosa vitu vingi.

Katika hatua nyingine, Kayuni ameitaka Serikali kudhamini michuano ya Taifa Cup, ambayo itasaidia kuibua vipaji vilivyojificha mikoani vitakavyolinufaisha Taifa.