Ijumaa , 13th Nov , 2020

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli amesema kipindi cha miaka mitano ijayo serikali yake itaboresha vitambulisho vya wajasiriamali ili kuwawezesha kupata mikopo.

Pichani mfano wa kitambulisho cha wafanyabiashara ndogo ndogo)

Rais Dk Magufuli ameyasema hayo leo bungeni jijini Dodoma wakati akizindua rasmi Bunge la 12 huku akilihutubia bunge hilo na Taifa kwa ujumla mabapo amesema kuwa lengo lake ni kuona kila mtanzania ananufaika na maendeleo ya ukuaji uchumi nchini.

“Tumekusudia kuboresha vitambulisho vya wajasiriamali, ikiwemo kuweka picha na taarifa muhimu kama ilivyo kwenye vitambulisho vya taifa, hii itawawezesha kutambulika, kukua na kutajirika na siyo siku zote wanabaki kuwa wafanyabiashara ndogo ndogo” amesema Rais Magufuli

Aidha Rais Magufuli amesema kuwa serikali yake itakazia programu za kukuza ujuzi na maarifa katika ujasisriamali kwa kutoa mafunzo kwa wajasirimali ili wawe na ujuzi ambao utawawezesha kuzalisha bidhaa zenye ubora na kuziuza ndani na nje ya nchi.