Jumatano , 30th Dec , 2020

Mbunge wa Makete Festo Sanga, amekabidhi na kuzifunga Solar panel tatu katika Zahanati ambazo aliahidi atawapatia wananchi wa Kijiji cha Ilindiwe, Kata ya Mang'oto, endapo watamchagua alipopita kuomba kura wakati wa kampeni za uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 28, 2020.

Mbunge wa Makete, Festo Sanga.

Akikabidhi Solar hizo, Mbunge Festo Sanga, amesema kuwa ameamua kuanza na suala la umeme wa jua kwenye Zahanati ya Kijiji hicho kwa sababu kiu kubwa kwa wananchi hao ilikuwa ni kupata umeme ili huduma za matibabu ziwepo hadi nyakati za usiku.

"Nilipokuja kuomba kura mliniambia hitaji lenu la kwanza ni umeme wa Solar kwenye Zahanati yenu hii, Zahanati hii inategemewa na sehemu kubwa ya wananchi wa Mang'oto, nimeona ni vyema nikaitekeleza mapema ili mama zetu wanapohitaji huduma ya uzazi waipate masaa yote pakiwa na umeme, nawaomba mzitunze solar hizi ili zitusaidie kwa muda mrefu wakati tunahangaikia umeme wa REA" amesema mbunge Sanga.

Baadhi ya Wananchi walioshuhudia utekelezaji wa ahadi hiyo wamesema, wameshangazwa na namna mbunge alivyotekeleza ahadi hiyo kwa uharaka kwa sababu ni ahadi ambayo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa kwanza wa mkoa wa Njombe na baadaye viongozi wengine lakini haikutekelezeka.