Jumatano , 14th Jul , 2021

Rais wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo ameshiriki kongamano la kumbukizi ya Rais wa Awamu ya Tatu Hayati Benjamini William Mkapa, ambapo pamoja na mambo mengine ameeleza ni kwa jinsi gani alivyoshuhudia uwezo wa Hayati Mkapa wakati wa machafuko yaliyotokea Zanzibar mwaka 2001.

Rais Samia Suluhu Hassan, akikabidhi tunzo ya picha kwa Mama Anna Mkapa kwa kutambua mchango wa Rais Mstaafu Hayati Benjamin Mkapa alioutoa kwa Taifa.

Kongamano hilo limefanyika hii leo Julai 14, 2021, Jijini Dar es Salam, na kuhudhuriwa na watu mbalimbali akiwemo na Mjane Mama Ana Mkapa, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Alhaji Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Kikwete, Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Mwinyi, na viongozi wengine mbalimbali pamoja na wageni walikwa.

"Sifa nyingine kubwa ya Mzee Mkapa ni uwezo wake mkubwa wa ya kuhimili ama kutokuogopa mijadala ya kimataifa sote tunakumbuka miaka 1990 na mwanzoni mwa 2000 kulikuwa na vuguvugu kubwa la kupinga masuala ya utandawazi, lakini yeye hakufuata mkumbo badala yake alijitokeza hadharani kuutetea na kueleza kwanini tunapaswa kuupokea," amesema Rais Samia.

Aidha, katika hotuba yake hiyo Rais Samia amesema kuwa katika kuandika kitabu chenye historia ya Tanzania hakiwezi kukamilika bila ya uwepo wa sura nzima ya Hayati Benjamin Mkapa kutokana na mageuzi makubwa aliyoyafanya kwa Taifa.