Jumanne , 17th Mei , 2022

Wadau wa bandari nchini wamesema kukamilika kwa upanuzi wa gati mbili za kisasa katika bandari ya Tanga kutasaidia watanzania kuacha kutumia bandari ya Mombasa Nchini Kenya. 

Wamesema  uwekezaji uliofanywa na serikali katika bandari ya Tanga, utaisaidia kuongeza mapato baada ya meli kubwa kufika kushusha mizigo.

Wakizungumza mara baada ya kutembelea bandari hiyo, wadau wanaohudhuria mkutano unaojadili changamoto zinazoikumba bandari hapa nchini, wamesema kuwa upanuzi wa gati katika bandari ya Tanga kutasababisha waweze kuhudumia meli kubwa.

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Wakala wa Meli nchini (TASAA) Daniel Malongo amesema mabadiliko yaliyofanyika yanaleta suluhisho la meli zilizokuwa zikishushia mizigo nchi jirani ya Kenya, zitafika katika banadari hiyo.

"Tulichokiona Tanga tunaweza kusema ni 'game changer'  kwamba kuna uwekezaji serikali imefanya, sasa naiona Tanga inakuwa suluhisho la mizigo iliyokuwa inapitia Mombasa, Meli kubwa  zitafika hapa na Revenue zetu zitakuwa juu," amesema Malongo.

Amesema matayarisho yaliyofanywa kwa ajili ya Kontena na mizigo mingine ambayo itasaidia kukuza uchumi kwa kuwa mapato yatapanda.

Naye Ofisa Sera, Mazingira wa Shirikisho la Viwanda nchini (CTI) Anna Kimaro amesema kwa maboresho yaliyofanywa na serikali yataleta fursa kwa wadau wanaosafirisha mizigo  kwenda nchi mbalimbali baada ya meli kubwa kufika bandari hiyo.

Amesema pia itaisaidia kupunguza msongamano na mlundikano wa mizigo katika bandari ya Dar es salaam na hivyo kuisaidia serikali kupata mapato.

Mkurugenzi wa Huduma za Uchukuzi Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Aron Kisaka amesema mradi wa maboresho ya Bandari katika kuhudumia mizigo hadi kufikia tani milioni tatu unaofanywa katika bandari hiyo utasaidia kufikia kina cha mita 13.

Amesema mradi huo ukikamilika utasaidia kupunguza mizigo inayohudumiwa katika bandari ya Dar es salaam hasa kwa wakazi wa mikoa ya Kaskazini na kwasasa watatumia muda mfupi kupitia bandari ya Tanga.

Awali meneja wa Bandari ya Tanga, mhandisi Masoud Mrisha amesema mradi huo ambao upo awamu ya pili ya utekelezwaji wake umefikia asilimia 45 na utarajiwa kukabidhiwa Novemba mwaka huu utakaokuwa na mita 450.