
Uamuzi huo umefikiwa jana Jumanne baada ya serikali ya jimbo la Baden-Württemberg kuidhinisha uhamisho wa umiliki wa sanaa hizo kwenda Nigeria, inayojumuisha eneo lililokuwa ufalme wa Benin hapo awali.
Akizungumza baada ya kikao cha baraza la mawaziri wa jimbo, waziri wa utamaduni wa jimbo la Baden-Württemberg Petra Olschowski amesema uamuzi huo sio tu wa kurejesha kazi hizo za sanaa, bali pia kutambua dhima ya jimbo hilo katika historia ya ukoloni.
Kazi hizo zilizoundwa kwa madini ya shaba zilitengenezwa mnamo karne ya 13, na zilitumika kama mapambo katika nyumba ya mfalme wa Benin.
Mapambo ya aina hiyo yapatayo 1,100 yanapatikana katika majumba 20 ya makumbusho nchini Ujerumani.