Ijumaa , 9th Jan , 2026

Mbinu hiyo ni miongoni mwa mipango kadhaa inayojadiliwa na Ikulu ya White House kuhusu kuipata Greenland, ikiwemo hata uwezekano wa kutumia jeshi la Marekani.

Maafisa wa Marekani wamejadili uwezekano wa kutuma malipo ya mkupuo kwa wakazi wa Greenland kama sehemu ya juhudi za kuwashawishi kujiondoa kutoka kwa Denmark na kujiunga na Marekani.

Ingawa kiasi kamili cha fedha na namna ya kukitoa bado haijafahamika, maafisa wa Marekani wakiwemo wasaidizi wa Ikulu ya White House wamezungumzia takwimu kati ya dola 10,000 hadi 100,000 kwa kila mtu.

Wazo la kuwalipa moja kwa moja wakazi wa Greenland, eneo la ng’ambo la Denmark, linaonyesha moja ya njia ambazo Marekani inafikiria kujaribu kutumia ili kukinunua” kisiwa hicho chenye watu takribani 57,000, licha ya msimamo wa mamlaka za Copenhagen na Nuuk kwamba Greenland haiuzwi.

Mbinu hiyo ni miongoni mwa mipango kadhaa inayojadiliwa na Ikulu ya White House kuhusu kuipata Greenland, ikiwemo hata uwezekano wa kutumia jeshi la Marekani.

Kwa upande wao, Viongozi wa Ulaya ikiwemo Ufaransa, Ujerumani, Italia, Poland, Hispania, Uingereza na Denmark yenyewe wametoa taarifa ya pamoja wakisema kuwa ni Greenland na Denmark pekee wenye mamlaka ya kuamua masuala yanayohusu uhusiano wao na kisiwa hicho wakijibu kauli za Trump na maafisa wengine wa White House, hasa kwa kuzingatia kwamba Marekani na Denmark ni washirika wa NATO waliofungwa na makubaliano ya ulinzi wa pamoja.

Trump kwa muda mrefu amesisitiza kuwa Marekani inahitajika kuipata Greenland kwa sababu mbalimbali, ikiwemo kuwa ina rasilimali za madini muhimu kwa matumizi ya kijeshi ya hali ya juu. Pia amesema kwamba nusu ya dunia ya Magharibi inapaswa kuwa chini ya ushawishi wa kijiografia wa Washington.

Ingawa majadiliano ya ndani kuhusu namna ya kuichukua Greenland yamekuwapo tangu kabla ya Trump kuingia madarakani mwaka mmoja uliopita, yamepata msukumo mkubwa baada ya serikali ya Trump mkamata kiongozi wa Venezuela, Nicolas Maduro, katika oparesheni ya ghafla.

Licha ya tafiti kuonyesha wengi wa Wagrinlandi wanataka uhuru, hofu kuhusu gharama za kiuchumi za kuachana na Denmark imewazuia wabunge wengi wa Greenland kuitisha kura ya maoni ya uhuru. Uchunguzi pia unaonyesha kwamba Wagrinlandi wengi, licha ya kuwa tayari kujitenga na Denmark, hawataki kuwa sehemu ya Marekani.