Thursday , 4th Jun , 2015

Serikali ya Tanzania imesema imeweka mpango maalumu wa ujenzi wa nyumba nafuu kwa waalimu ili kuweza kusaidia katika ufanisi wao na kuinua kiwango cha elimu nchini.

Akijibu maswali bungeni mjini Dodoma leo naibu waziri wa TAMISEMI Kassimu Majaliwa amesema kuwa serikali bado haijaweza kutekeleza miradi ya ujenzi wa nyumba za waalimu katika maeneo ya mjini na vijijini lakini mpaka sasa serikali imeweka mpango wa kuwahusisha wabia ili kusaidia upatikanaji wa makazi ya kudumu kwa walimu na watumishi wengine wa serikali.

Amesema bilioni 67.2 kwa ajili ya ujenzi wa shule 528 zikiwemo nyumba za walimu 228 na mpaka sasa halmashauri 40 zimekwishapatiwa fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu ambazo zitasaidia katika jitihada za kufikia malengo katika kuboresha elimu.

Aidha naibu waziri wa fedha Mh. Mwigulu Nchemba amesema wizara yake imekwisha peleka kiasi cha shilingi bilioni 10 kwaajili ya kuwasaidia kujikimu walimu waliopata ajira mpya na kupangiwa mahali pa kazi na kuitaka wizara husika kuhakikisha wanaandaa malipo ya walimu kabla hawajafika vituo vya kazi ili kuondoa usumbufu.