Tuesday , 26th Aug , 2014

Serikali ya Tanzania imesema upanuzi wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam ambao utajulikana kama terminal three, utakamilika na kuanza kutumika mwezi Oktoba mwakani.

Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi nchini Tanzania Dkt Shaaban Mwinjaka.

Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi Dkt Shaaban Mwinjaka, amesema hayo jijini Dar es Salaam leo wakati wa kongamano la kimataifa la uwekezaji katika miundombinu ya reli na barabara, kongamano lililoandaliwa na taasisi kutoka nchini Indonesia ya Magenta Global na kukutanisha wadau wa uchukuzi na uwekezaji kutoka ndani na nje ya bara la Afrika.

Dkt Mwinjaka amesema mara itakapokamilika, sehemu iliyopanuliwa katika uwanja huo itatumika kwa ajili ya safari za ndege za kimataifa wakati viwanja viwili vilivyokwepo awali vitatumika kwa ajili ya safari za ndege za ndani ya nchi.

Aidha, Dkt Mwinjaka amesema wizara yake imeanza kufanya upembuzi yakinifu kuangalia uwezekano wa kupanua maeneo yanayofikiwa na usafiri wa reli katika jiji la Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Dkt Mwinjaka, hatua hiyo inalenga kupunguza tatizo la msongamano wa magari katika barabara za jiji la Dar es Salaam, tatizo linalochangiwa na ufinyu wa miundombinu ya usafiri.

Katibu Mkuu huyo ameyataja maeneo wanayofikiria kufikisha usafiri wa reli kuwa ni kati ya Mwenge na Bagamoyo kupitia Tegeta na Bunju, Barabara ya Morogoro kuanzia Ubungo hadi Kibaha pamoja na maeneo yaliyo katika barabara ya Kusini.