Saturday , 29th Dec , 2018

Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya amethibitisha kukamatwa kwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, Dkt Vincent Mashinji pamoja na viongozi wengine watatu kwa makosa ya kufanya kusanyiko bila kibali.

Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya, Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, Dkt Vincent Mashinji

Viongozi wengine waliokamatwa ni Katibu wa CHADEMA Mkoa wa Kilimanjaro, Basir Lema, Mwenyekiti wa halmashauri ya Hai, Egra Mchomvu na msaidizi wa mbunge wa Hai, Irine Lema.

Mkuu wa Wilaya ya Lengai Ole Sabaya amesema "ni kweli tumemkamata Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Mashinji, Katibu wa CHADEMA Mkoa wa Kilimanjaro, Basir Lema, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Hai, Egra Mchomvu na msaidizi wa mbunge wa Hai, Freeman Mbowe, Irine Lema kwa kufanya mkusanyiko usio halali"

Aidha Sabaya amesema kuwa "naomba nitoe wito kwa wanasiasa kuheshimu sheria na taratibu, kama mnataka mkutano kuna taratibu hamuwezi kuvamia na kufanya mikutano kiholela"

Taarifa za kukamatwa kwa Katibu Mkuu CHADEMA zilianza kusambaa kupitia mitandao ya kijamii ambapo www.eatv.tv ilijaribu kuwatafuta baadhi ya viongozi wa CHADEMA ili kufahamu juu ya hatua watakazozichukua lakini simu zao ziliita bila majibu yeyote.