
Kamishna Simon Sirro
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro, amesema kuwa tukio hilo limetokea majira ya saa 3 asubuhi ambapo watuhumiwa hao wa ujambazi wakiwa na silaha aina ya MARK IV, ikiwa imekatwa kitako chake, wakiwa na pikipiki MC 787 BEP BOXER rangi nyeusi.
Kamishna Sirro amesema kuwa majambazi hao walianza kufyatua risasi hovyo baada ya kugundua kuwa walikuwa wakifuatiliwa na askari wa kikosi maalum cha kupambana na ujambazi na ndipo askari walipoanza kujibu mashambulizi na kuwajeruhi wote wawili na kuchukua silaha yao, kisha majambazi hao kukimbizwa Hospitali ya Muhimbili kwa matibabu.
Amesema kuwa taarifa za awali za jeshi hilo zinaonesha kuwa watu hao walikuwa wamepanga kuvamia kiwanda kimojawapo katika eneo hilo na kwamba upelelezi bado unaendelea.
Katika hatua nyingine, jeshi hilo limewakamata watuhumiwa 87 kwa makosa mbalimbali ya uhalifu baadhi yao wakiwa na pombe haramu ya gongo lita 148, bhangi kete 95 na puli 48.
Watuhumiwa hao walikamatwa katika msako maalum uliofanyika maeneo ya Mbagala, Buguruni, Kiluvya, Gongo la Mboto, Tandika, Ukonga, Banana, Kunduchi, Kawe na keko kwa makosa mbalimbali ikiwemo kuvunja nyumba usiku na kuiba, kuvuta na kuuza bhangi, kuuza na kunywa gongo, kupiga debe, uzembe na uzururaji na kwamba wote watapelekwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.
Sirro pia amewatahadharisha wananchi juu ya uwepo wa watu wanaofanya utapeli kwa kujifanya kuwa ni watu wanaotafutia watu ajira, kwa kuchukua pesa zao.
Kwa upande wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Sirro amesema kuwa Polisi Dar es Salaam imekusanya shilingi milioni 541.83 kutokana na makosa ya barabarani kuanzia tarehe 3/10/2016 hadi 9/10/2016.