Wednesday , 21st Jan , 2015

Wenyeviti watatu wa Kamati za Bunge waliotajwa katika sakata la Escrow tayari wamejiuzulu nafasi hizo kwa mujibu wa maazimio ya Bunge na nafasi zao zinashikiliwa na makamu wenyeviti wa kamati hizo..

Akithibitisha taarifa hizo Spika wa Bunge Mh. Anna Makinda amesema kuwa kwa mujibu wa maazimio ya Bunge, wenyeviti hao walipaswa kuwajibika mara moja katika kamati zao, na kwamba sio jukumu lake kuwaondoa katika nafasi hizo kwa kuwa walichaguliwa katika kamati zao.

Amesema yeye anapokea taarifa kutoka ndani ya kamati kuhusu uwepo wa mwenyekiti au la, ili atoe ruhusa ya kufanyika kwa uchaguzi wa mwenyekiti mpya lakini anachojua ni kwamba hadi sasa wenyeviti hao tayari wamejiuzulu nafasi hizo.

Wenyeviti hao ni Wiliam Ngeleja aliyekuwa mwenyekiti wa Kamati ya Sheria, Katiba na Utawala aliyetajwa kupokea pesa kutoka kwa James Rugemalira, Andrew Chenge aliyekuwa mwenyekiti wa kamati ya Bajeti ambaye pia anatajwa kupokea fedha kiasi cha shilingi Bilion 1.6 kutoka kwa James Rugemalira.

Mwingine ni Victor Mwambalaswa aliyekuwa mwenyekiti wa kamati ya Nishati na Madini ambaye pia alikuwa katika bodi ya TANESCO inayodaiwa kuhusika kwa kiasi kikubwa katika sakata la fedha zilizokuwa katika akaunti ya Tegeta Escrow.

Taarifa kutoka ndani ya kamati ya bajeti zinasema kuwa Andrew Chenge alijiuzulu mapema nafasi yake ambapo kwa hivi sasa kamati hiyo iko chini ya makamu mwenyekiti Bulugu Festus Limbu