
Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini Esther Matiko.
Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko wamerudishwa gereza la Segerea baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es salaam kusimamisha usikilizaji wa rufaa yao hadi pale rufaa ya serikali itakapo amriwa.
Serikali imekata rufaa Mahakama ya rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama ya Kuu kusikiliza rufaa ya wawili waliyoiwasilisha mahakamani hapo kupinga Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwafutia dhamana Novemba 23, 2018.
Baada ya uamuzi wa Jaji Sam Rumanyika anayesikiliza rufani hiyo ya Mbowe na Matiko kutoa uamuzi huo leo jioni Ijumaa Novemba 30, 2018 Mbowe aliwasalimia wafuasi wa chama chake waliofurika mahakamani hapo kuwa ‘People’s nao wakaitikia 'Power', nakumalizia kwa kuwaeleza, "mapambano yanaendelea".
Jaji Rumanyika amekubaliana na hoja za Serikali kuwa uamuzi mdogo hauwezi kumaliza shauri hauwezi kukatiwa rufaa na wadaiwa wengine isipokuwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) tu.
Jaji Rumanyika amesema DPP anapewa mamlaka ya kukata rufaa kwa uamuzi mdogo chini ya kifungu cha 6 cha Sheria ya Mamlaka ya Rufaa. Kuhusu taarifa ya kusudio la kukata rufaa Mahakama ya Rufani, amesema hilo liko wazi kwamba kunapokuwepo na taarifa hiyo mahakama ya chini haiwezi kuendelea na shauri.
"Hivyo mwenendo wa shauri hili unasimama hadi rufaa iliyokatwa Mahakama ya Rufani itakapoamriwa," amesema Jaji Rumanyika.
Serikali imekata rufaa katika Mahakama ya Rufani, ikipinga uamuzi wa Mahakama Kuu kukubali kuendelea na usikilizwaji wa rufaa ya kina Mbowe.
Wawili hao walifutiwa dhamana hiyo Novemba 23, na Hakimu Mkazi Mkuu Wilbard Mashauri, kufuatia maombi ya upande wa mashtaka, kwa madai ya kukiuka masharti ya dhamana kwa kutokufika mahakamani tarehe ambazo kesi yao ilipangwa kwa ajili ya usikilizwaji wa awali.
Baada ya kufutiwa dhamana hiyo walikata rufaa Mahakama Kuu, kupinga uamuzi huo wa kufutiwa dhamana. Kabla ya rufaa hiyo kusikilizwa serikali iliweka pingamizi la awali ikiomba mahakama iitupilie mbali rufaa hiyo, ikidai ina kasoro za kisheria.
Mahakama Kuu licha ya kukubaliana na baadhi ya hoja za pingamizi la Serikali lakini imezikataa hoja nyingine ambazo zingeweza kusababisha rufaa hiyo kutupiliwa mbali kama ingezikubali. Hivyo ikaamua kuendelea na usikilizwaji wa rufaa hiyo.