Tuesday , 20th Nov , 2018

Mbunge wa Jimbo la Kilwa Kusini Selemani Bungara “Bwege” amefunguka juu ya mazungumzo yake na Mbunge wa Tandahimba Katani Katani yalivyopelekea mbunge mwenzake kubadilisha msimamo wa kuhamia Chama Cha Mapinduzi.

Mbunge wa Tandahimba Katani Katani.

Kauli hiyo ya Mbunge Bwege imekuja kufuatia tetesi zilizozagaa wiki iliyopita zikimtaja Mbunge wa Jimbo la Tandahimba, Katani Katani kutaka kuhamia Chama cha Mapinduzi CCM kutoka CUF.

Akizungumza na www.eatv.tv Mbunge Bwege amekiri kuzungumza na Mbunge huyo siku ambayo Mbunge wa Temeke Abdallah Mtolea alitangaza kukihama chama chake cha CUF.

Mheshimiwa Katani alinambia yeye ahami, lakini nilimfuata kumuuliza kuhusu kuhamia CCM akanijibu hawezi kuhama, kama kumshawishi,  nilimshawishi kwa njia hiyo japo tuliongea kwa muda mrefu na nikaongea kwa muda mrefu sana kuanzia saa 7 hadi saa 11,” amesema Selemani Bungala.

Na Kwa mujibu wa maelezo yake alivyotoka kwangu kabla ya kwenda bungeni alinambia anaenda kwa Mbunge wa Vunjo James Mbatia japo sikujua alizungumza nini, ila baada ya hapo alikanusha bungeni kuwa hawezi kuhama chama,” ameongeza.

Novemba 15 mwaka huu ikiwa ni siku ya mwisho ya Chama Cha Mapinduzi kuwapokea Mbunge mmoja wa Chama Cha Wananchi CUF Abdallah Mtolea alitangaza kujiuzulu nafasi yake na baadaye kutangaza kujiunga na Chama Cha Mapinduzi.