Thursday , 15th Jan , 2015

MFANYABIASHARA wa kuuza samaki, Mkome Marwa (39) wa mtaa wa Nyasura wilayani Bunda, ameuawa na watu wasiojulikana baada ya kupigwa risasi njiani akiwa na mke wake, huku mwingine akijeruhiwa katika matukio mawili tofauti wilaya humo.

Kamanda wa polisi mkoa wa Mara, Phillipo Kalangi.

Kamanda wa polisi mkoa wa Mara, Phillipo Kalangi, amesema tukio la kwanza limetokea Januari 12 mwaka huu, saa 3 usiku, eneo la Nyasura wakati Marwa akiwa na mkewe wakirejea nyumbani kwao, amepigwa risasi na mtu asiyefahamika.

Hata hivyo, Kilangi amesema mtu huyo baada ya kufanya tukio hilo hakuweza kuchukua kitu chochote kwa mfanyabiashara huyo aliyefariki hospitali ya rufaa Bugando, Mwanza wakati akipatiwa matibabu, huku ofisi yake ikituma makachero wilayani humo kufanya uchunguzi wa kina.

Amesema baada ya mfanyabiashara huyo kupigwa risasi, akajikokota hadi nyumba ya jirani walikojifungia ndani ya geti na mkewe, hali iliyomfanya muuaji kuwafuata tena lakini alipokuta geti limefungwa, akaondoka zake.

Tukio la pili amesema limetokea siku hiyo saa 4:00 eneo la Bunda Day, wakati mwanaume mmoja, Ndaro Malemi (25), aliyekuwa anaelekea nyumbani kwake, alijeruhiwa kwa risasi na mtu asiyefahamika ambaye pia hakuchukua kitu chochote.

Malemi aliyelazwa katika hospitali ya DDH-Bunda, alisema mtu huyo aliyevaa koti jeusi alimvizia njiani na kumwamuru atoe kila kitu na baada ya kukimbia ndipo alipomiminiwa risasi mbili na kutokomea zake kusikojulikana.

Daktari wa zamu katika hospitali hiyo, Dk. Amosi Manya, amesema waliwapokea majeruhi wawili hospitalini hapo lakini mmoja alikuwa na hali mbaya na kukimbizwa Bugando lakini alifariki akiwa anapatiwa matibabu.