Monday , 27th May , 2019

Ikiwa ni siku tatu zimebaki kabla ya sheria mahsusi ya kuzuia matumizi ya mifuko ya plastiki, tayari mifuko mbadala imeanza kusambaa katika mitaa mbalimbali jijini Dar es salaam.

Wakazi wa Dar es salaam wakiwa na mifuko mbadala

Maeneo ya Mwenge jijini Dar es salaam baadhi ya wakazi wameonekana na mifuko hiyo, mingi ikiwa imetengenezwa kwa karatasi ngumu pamoja na vitambaa laini imeanza kutumika na mingine ikitangazwa kuuzwa katika mitandao ya kijamii kwa yeyote anayehitaji kuipata.

Kwa wauzaji wa mifuko hiyo katika mitandao ya kijamii wameigawanya katika sehemu mbalimbali, ambapo kwa wenye uhitaji wa jumla ni kwamba seti ndogo yenye mifuko 100 kama inavyoonekana kwenye picha inauzwa 18,000 TZS, seti ya kati ikiuzwa kwa 24,000TZS, seti kubwa ikiuzwa kwa 28,000TZS na seti ya mifuko mifuko mikubwa zaidi ikiuzwa kwa 36,000TZS.

Mei 23, Waziri wa Ofisi ya Rais, Muungano na Mazingira, Mhe. January Makamba aliandika katika ukurasa wake rasmi wa Twitter kuwa ifikapo Juni 1 na kuendelea, ukaguzi utafanyika nchi nzima madukani, masokoni, magengeni, viwandani, mipakani na sehemu nyingine zinakouzwa bidhaa kuhakikisha kwamba matumizi ya mifuko ya plastiki yamekoma. 

Pamoja na hayo pia, Mei 25 alitoa mwongozo wa namba za bure za simu za kupiga, kutuma SMS na Whatsapp kwa walio na maswali, maoni, ushauri au taarifa yoyote kuhusu katazo la mifuko ya plastiki, zoezi linaloanza leo Jumatatu, Mei 27.

Hata hivyo licha ya tarehe ya kuanza kutumika kwa katazo hilo kukaribia, baadhi ya wauza maduka na wananchi wameendelea kutumia na wengine hata katika mikusanyiko ya watu.