Thursday , 9th Jun , 2016

Mbunge wa Newala mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mhe. George Mkuchika, ameshinda kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa ubunge iliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea ubunge wa jimbo hilo kupitia Chama cha Wananchi (CUF) Juma Manguya.

Mbunge wa Newala mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mhe. George Mkuchika,

Ushindi huo umetokana na maamuzi ya mahakama kuu kanda ya Mtwara kutupilia mbali kesi hiyo ambayo ilikuwa ikisikilizwa katika mahakama ya wilaya ya Newala, ambapo hukuku iliyosomwa na Jaji wa mahakama kuu ya Tanga, Amour Khamis ilisema mlalamikaji ameshindwa kuthibitisha katika kesi yake kwa kiwango stahiki kwamba uchaguzi huo haukuendeshwa kwamujibu wa sheria.

Akizungumza baada ya hukumu hiyo, wakili wa Manguya, Rainery Songea, amesema hajakubaliana na maamuzi hayo na kwamba taratibu zimeanza kufanyika ili kuweza kukata rufaa lakini kwanza atahitaji apate nakala ya hukumu iliyosomwa na Jaji, huku mteja wake akiunga mkono suala hilo.

Kwa upande wake, wakili wa kujitegemea aliyekuwa akimsimamia George Mkuchika, Hussein Mtembwa, amesema kazi yake ilikuwa ni kuhakikisha haki inatendeka katika katika kipindi chote cha kesi hiyo jambo ambalo limefanikiwa, huku mteja wake akiahidi kuwatumikia wananchi wa jimbo lake bila ubaguzi.

Hata hivyo, mahakama hiyo imetoa nafasi ya kukata rufaa kwa mtu yoyote ambaye hatokubaliana na maamuzi yaliyoamriwa.