Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan akihutubia katika mahafali
Samia ametoa kauli hiyo katika hotuba yake kwenye mahafali ya pili ya Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika (EASTC) Jijini Dar es Salaam na kuziagiza wizara, idara na taasisi za serikali kuimarisha matumizi ya takwimu sahihi kwa ajili ya kupanga na kuweka mikakati ya kuwaletea wananchi maendeleo endelevu.
Ameutaka uongozi wa Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika uimarishe ushirikiano na Wakuu wa Takwimu wa Afrika kwa kuhakikisha watakwimu wanaoingia katika soko la ajira wanafanya kazi zao kwa kufuata misingi ya kisheria na kanuni zake katika ukokotoaji wa takwimu zinazokubalika kitaifa na kimataifa ambazo zitawezesha Afrika kupanga maendeleo ya wananchi kwa ufanisi mkubwa.
Amewahimiza wahitimu wa Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika pindi watakapoanza kufanya kazi zao wafanye kazi kwa ufanisi na kwa umakini wa hali ya juu ili kutimiza azma ya kutokomeza kabisa umaskini uliokithiri ifikapo mwaka 2030 katika bara la Afrika.
“Wito wangu kwa Wizara, Idara na Taasisi za Serikali kuhakikisha zinaimarisha vitengo vya takwimu kwa kuwaruhusu maofisa waliopo katika vitengo vyao vya sera na mipango wapate fursa ya kupatiwa mafunzo elekezi na ya muda mfupi kwa ajili ya kuongeza ujuzi wao wa kuchambua na kukokotoa takwimu rasmi”
Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan akiwa na mabalozi wa nchi mbalimbali waliohudhuria mahafali
Kwa upande wake, Waziri wa Fedha na Mipango Dkt Philip Mpango amesema serikali itaendelea kushirikiana kikamilifu na Ofisi ya Taifa ya Takwimu katika kutumia takwimu sahihi ambazo zimetolewa na ofisi hiyo katika kupanga shughuli za maendeleo za taifa.
Katika mahafali hiyo Makamu wa Rais amewatunuku vyeti wahitimu 133 katika ngazi za Shahada ya Uzamili ya Takwimu, Shahada ya awali ya takiwmu na Stashahada ya takwimu kwa wahitimu kutoka nchi kumi za Afrika ambazo ni Nigeria,Ghana,Sierra Leon, Ethiopia,Somalia, Uganda, Swaziland, Liberia, Rwanda na mwenyeji Tanzania.
