Monday , 10th Oct , 2016

Serikali imesema hakuna uhaba wa dawa nchini kwa sasa kama inavyoendelea kuuenezwa na baadhi ya watu na kusisitiza kuwa habari hizo ni za upotoshaji na zinalenga kuwatisha wananchi.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu

Kauli hiyo imetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu wakati akitolea ufafanuzi ripoti mbalimbali ambazo zinatolewa na baadhi ya taasisi zisizo za kiserikali zinazoonesha kuwepo kwa uhaba wa dawa na vifaa tiba nchini.

Akifafanua zaidi kuhusu suala hilo Mhe Mwalimu amesema ni kweli kulikuwa na uhaba wa chanjo zinazotolewa kwa watoto wadogo na siyo uhaba wa dawa zote kwa ujumla.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mkuu wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD) Bw. Laurean Bwanakunu amesema wameanza kubaini vituo vya afya ambavyo vilikuwa na upungufu wa dawa na chanjo tayari kwa kupeleka dawa hizo kwa kuwa bohari ya dawa ina dawa za kutosha.