Wednesday , 8th Feb , 2017

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamisha Simon Sirro amesema kuwa jeshi hilo linaendelea kumshikilia msanii wa filamu nchini Wema Sepetu hadi pale uchunguzi utakapo kamilika.

Akizungumza leo na wanahabari, Kamishna Sirro amesema jeshi hilo linaendelea na uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazomkabili msanii huyo, ikiwa ni pamoja na kuchunguza vielelezo alivyokutwa navyo kwa kutumia ofisi ya Mkemia Mkuu, ili kujiridhisha kama kweli zile ni dawa za kulevya, na uchunguzi huo ukikamilika, atafikishwa mahakamani.

Pia Sirro amesema jeshi hilo linawashikia jumla ya watu 85 waliokamatwa kwa kipindi cha siku 3 kwa tuhuma za kujihusisha na matumizi ya dawa za kulevya, na kufafanua kuwa watu hao ni tofauti na wale 112 waliotajwa juzi.

Taarifa hiyo inamaanisha kuwa hadi sasa Jeshi hilo limekamata watu 197 kwa tuhuma hizo.

Aidha, Kamisha Sirro amewaonya watu wanaotoa taarifa za uongo kwa jeshi hilo kuhusu dawa za kulevya kuwa endapo watabainika kusema uongo na kutaja jina la mtu asiye jihusisha na shuguli za dawa za kulevya atachukuliwa hatua za kisheria.

Kuhusu mbunge Tundu Lissu, Sirro amesema, bado wanaendelea kumshikilia Mbunge huyo wa Singida Mashariki kwa tuhuma za kutumia lugha za uvunjifu wa amani na atafikishwa mahakama mara baada ya uchunguzi dhidi yake utakapokamilika.

Tundu Lissu