Tuesday , 11th Oct , 2016

Mawaziri wa Fedha na Magavana kutoka nchi mbalimbali za kiafrika, wanachama wa benki ya dunia na shirika la fedha la kimataifa wamezitaka taasisi hizo kuweka mipango inayoakisi na kutatua changamoto zinazolikabili bara la Afrika.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango (kulia) akisalimiana na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia anayeshughulikia Kanda ya Afrika.

Viongozi hao wanashughulikia sekta ya fedha barani Afrika wametoa kauli hiyo Washington DC nchini Marekani ambapo wametaja changamoto hizo ni pamoja na uhalifu, umasikini, mizozo ya kivita na majanga yanayotokana na mabadiliko ya tabia nchi.

Aidha viongozi wamezitaka taasisi hizo kuweka uwiano wa uwakilishi wa uongozi wa juu ili kuhakikisha maslahi mapana ya nchi hizo yanalindwa na maendeleo endelevu ya nchi hizo yanafikiwa kwa haraka.

Akizungumza katika moja ya mikutano hiyo Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango, amesema mashirika hayo ya fedha ya kimataifa ya mchango mkubwa kwa maendeleo ya nchi za kiafrika ikiwemo Tanzania.

Dkt. Mpango amesema kuwa uchumi wa Tanzania unakuwa kwa kasi kwa wastani wa asilimia 7 kwa mwaka lakini changamoto kubwa iliyopo ni kuhakikisha kuwa uchumi huo unaonekana katika maisha ya kawaida ya wananchi wake.