Friday , 22nd Dec , 2017

Shirika la Umeme Tanzania TANESCO kupitia kwa Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi Dkt. Alexander Kyaruzi,  limewahakikishia Umeme wa uhakika wakazi wa Mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma.

Dkt. Kyaruzi amewahakikishia hilo wakati wa ziara yake ya kikazi katika mikoa hiyo, akiambatana na wajumbe wengine wa bodi pamoja na viongozi waandamizi wa TANESCO Makao Makuu na Kanda ya Kusini.

Akiongea na wananchi pamoja na viongozi wa Serikali Mkoani Lindi, Dkt. Kyaruzi amesema tayari TANESCO imefanya matengenezo makubwa katika mitambo ya kuzalisha umeme wa Gesi wa Megawati 18. Mtambo huo unahudumia Mikoa ya Mtwara pamoja na Baadhi ya maeneo ya Lindi kupitia laini mpya ya 132kV Mtwara-Mahumbika.

Aidha Dkt. Kyaruzi ameeleza kuwa mradi huo uliojengwa na  mafundi wazawa kutoka ndani ya TANESCO kupitia kampuni Tanzu iitwayo ETDCO umekamilika tangu mwezi Julai mwaka huu.

Kwa upande wa wananchi wa maeneo hayo wameonesha kufarijika na kupata shauku kubwa ya kuunganishwa na kuboreshewa huduma za umeme ili kuwezesha kufanyika kwa wepesi kwa shughuli zao mbalimbali za maendeleo.