Friday , 2nd Sep , 2016

Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) imeendelea na zoezi la uhakiki wa wamiliki wa namba za utambulisho wa mlipa kodi (TIN) na kusisitiza kuwa zoezi hilo linafanyika bure na kwamba wamiliki wake hawatakiwi kulipia gharama yoyote.

Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Alphayo Kidata (pichani) hivi karibuni alizindua zoezi hilo la uhakiki litakalodumu kwa muda wa siku sitini.

Mkuu wa Kituo cha Uhakiki kilichopo jengo la Millenium Tower jijini Dar es Salaam Bi. Evelyne Lwendo, ameiambia EATV kuwa katika zoezi hilo, wamebaini changamoto kadhaa mojawapo ikiwa ni kuibuka kwa watu wenye TIN ambazo hazijatumika kwa muda mrefu.

Kwa mujibu wa Bi. Lwendo kwa ujumla bado mwamko umekuwa mdogo kwa watu wanaokwenda kufanya uhakiki na kwamba amewatoa hofu wananchi kuwa zoezi hilo halina mpango wowote wa kuwatoza fedha zaidi badala yake linalenga kuwa na idadi kamili pamoja na kuboresha mfumo wa usajili wa namba za mlipa kodi.