Msemaji wa Idara ya Uhamiaji Ally Mtanda amesema watu hao tisa wamekamatwa jana kwa tuhuma za kuzuia maofisa wa idara hiyo wasitimize majukumu yao na kwa sasa wanawahoji.
"Watu hao baada ya maofisa wetu jana kufika pale KIU waliamua kuwazuia kwa kufunga milango ili tusipate nafasi ya kufanya kile ambacho kimetupeleka,"amesema.
Kukamatwa kwa watu hao kunafanya idadi ya wanaowashikiliwa na Idara ya Uhamiaji kufikia 48.
"Idara ya Uhamiaji inaendelea kuwahoji na kati ya hao wanaoshikiliwa wapo raia wa Nigeria watano, raia wa Congo mmoja, raia wa Uganda 30, raia wa Kenya 3 pamoja na hao raia wa Tanzania 9,"amesema.
Amefafanua Idara ya Uhamiaji itaendelea kukagua vyuo mbalimbali nchini kwani ni agizo la Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.