Jumanne , 14th Mei , 2024

Tanzania imeongoza kikao cha wataalamu kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika kujadili kuhusu vipaumbele vya sera katika masuala ya nishati safi ya kupikia ili kuja na azimio litakalopitishwa na wakuu wa nchi husika barani humo.

Kikao hicho kimefanyika katika ofisi za shirika la nishati la kimataifa (International Energy Agency - IEA), jijini Paris, Ufaransa ikiwa ni sehemu ya vikao mbalimbali kuelekea Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Nishati Safi ya Kupikia kwa Afrika utakaofanyika tarehe 14 Mei 2024 jijini humo.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa kikao na Mshauri wa Rais wa Tanzania wa Masuala ya Mazingira Dkt. Richard Muyungi, kikao hicho kimelenga kujadili masuala yote ya msingi na ya kipaumbele kwa kila nchi ili azimio litakalofikiwa liweze kutekelezeka.

"Kupitia kikao hiki tunataka utekelezaji wa azimio tutakalokuja nalo juu ya masuala ya nishati safi ya kupikia uendane na matakwa ya kila nchi kwa kuzingatia Programu ya Nishati Safi ya Kupikia itakayosaidia Wanawake Barani Afrika (AWCCSP) na mikakati mbalimbali ya agenda husika," ameeleza Dkt. Muyungi.

Azimio hilo lililojadiliwa linatarajiwa kupitishwa rasmi na wakuu wa nchi katika Mkutano husika ili lianze kutumika kama dira na ahadi ya kila nchi barani Afrika katika kutekeleza masuala ya nishati safi ya kupikia.

Kikao hicho kimehudhuriwa na wataalamu kutoka nchi zaidi ya 40, huku Tanzania ikiwakilishwa na viongozi kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais akiwemo Naibu Katibu Mkuu Bi. Christine Mndeme, Mkurugenzi wa Mazingira Bi. Kemilembe Mutasa na wataalamu kutoka Wizara ya Nishati na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuhutubia na kuongoza mkutano huo kama Mwenyekiti Mwenza akishirikiana na wenyeviti wenzie watatu ambao ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kimataifa ya Nishati, Dkt. Fatih Birol; Waziri Mkuu wa Norway, Mhe. Jonas Støre na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Akinwumi Adesina