
Baadhi ya wafuasi wa CHADEMA, wakizuiliwa na polisi Mahakama kuu kanda ya Dar es salaam.
Kabla ya kuwatawanya wafuasi hao, Jeshi la Polisi liliwataka wafuasi kutojihusisha na matendo yoyote yatakayotishia hali ya utulivu mahakamani hapo, jambo ambalo ilikuwa ngumu kutokana na idadi kubwa ya watu waliofika kwenye kesi hiyo.
Aidha jeshi hilo liliwakataza wafuasi hao kutoimba nyimbo zozote mahakamani hapo, pamoja na kuwapiga marufuku kuingia ndani ya jengo la mahakama, jambo ambalo lililamikiwa na baadhi ya wafuasi yao.
Mahakama kuu Kanda ya Dar es salaam leo inatarajiwa kutoa uamuzi wa mapingamizi, juu ya madai yaliyotolewa na upande wa Jamhuri juu ya kutosikilizwa kwa shauri la rufaa kwa mtuhumiwa Freeman Mbowe pamoja na Esther Matiko.
Novemba 23 mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, iliwafutia dhamana wabunge hao wawili baada ya kujiridhisha, kuwa Mbowe na Matiko walikiuka taratibu za dhamana.