Friday , 28th Dec , 2018

Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo) na kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe amemuomba Rais Dkt. Magufuli kusikiliza pia maombi yao kuhusiana na nyongeza ya mshahara pamoja na muswada wa vyama vya siasa.

Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo) Zitto Kabwe.

Zitto kupitia ukurasa wake wa twitter amesema kuwa Rais pia awasikilize kuhusiana na madai ya wadau wa korosho pamoja na kero nyingine na asiishie kwenye kikokotoo cha mafao ya hifadhi ya jamii pekee.

"Rais Magufuli atusikilize pia kuhusu mishahara ya watumishi  wa umma, atusikilize kuhusu mateso  ya wadau wa korosho na atusikilize kuhusu muswada wa sheria ya vyama vya siasa", ameandika Zitto Kabwe.

Zitto ameongeza kuwa, "Kwetu huu si wakati wa kunyang'anyana sifa. Washindi ni wafanyakazi na Watanzania. Tunapoelekea mbele, tunamuomba Rais Magufuli asiwe na aibu kutusikiliza na mengine mengi kwa kuwa  nia yetu ni njema tunajenga nchi moja".

Mapema leo Rais Magufuli, ameagiza vikokotoo vya mafao ya wafanyakazi katika mifuko ya hifadhi ya jamii, vilivyokuwa vinatumika kabla ya mifuko kuunganisha viendelee kutumika kwa kila mfuko hadi mwaka 2023.