Friday , 30th Nov , 2018

Umoja wa Mataifa (UN) umeongeza tamaduni ya muziki wa reggae kwenye hazina za kiutamaduni za dunia, ambazo zinahitajika kulindwa na kutangazwa zaidi.

Hatua hiyo imefikiwa hivi karibuni baada ya ombi la muda mrefu kutoka nchi ya Jamaica ambalo liliwasilishwa na waziri wake wa utamaduni, Olivia Grange , katika mkutano wa Umoja wa Mataifa kutaka kuutambuliwa rasmi kwa muziki huo.

Kutokana na hilo, UNESCO imesema kwamba mchango wa muziki huo kimataifa ukijadili issue mbali mbali za haki, upinzani, upendo na utu, umeleta nguvu kwenye ufahamu wa ubongo, siasa za jamii pamoja na hisia na kiroho.

Muziki wa reggae sasa utaungana na tamaduni zingine duniani ambazo zimetambuliwa na Umoja wa Mataifa, ukiwemo mchezo wa Hurling , ujenzi wa ukuta kwa mawe matupu na nyinginezo.

Muziki wa reggae uliasisiwa miaka ya 1960 baada ya kuunganishwa kwa mapigo ya muziki wa aina ya Ska na Rock stead, ambapo ulianza kujulikana kwa watu kupitia bendi ya muziki ya 'Toots and the Maytals', kisha The Wailers iliyoanzishwa na Bob Marley, Peter Tosh na Bunny Wailers kushika hatamu na kuzidi kuupeleka muziki wa reggae kimataifa, kwa ngoma zao kali zenye ujumbe wa amani, upendo na umoja.

Muziki wa reggae umeacha alama kubwa duniani kutokana na jumbe zake, ikiwemo wimbo wa Afrika Unite, ambao ulikuwa ni moja ya ndoto za wapigania uhuru wa bara la Afrika na kuanzishwa kwa Umoja wa Afrika (AU).

Mpaka sasa muziki huo unaendelezwa na wanamuziki mbali mbali duniani, huku Jamaica ikibaki kuwa kitovu cha muziki huo ambao una uwezo mkubwa wa kubadilisha fikra za binadamu na kuhamasisha amani, upendo, umoja na usawa wa haki.