Monday , 26th Nov , 2018

Klabu ya Alliance ya mkoani Mwanza imemtambulisha kocha mpya pamoja na wasidizi wake, ikiwa ni wiki kadhaa baada ya aliyekuwa kocha wake mkuu, Papii Kailanga kuachana na klabu hiyo.

Viongozi wa Alliance wakimtambulisha kocha mkuu, Malale Hamsini

Alliance imemtambulisha kocha, Malale Hamsini aliyetokea klabu ya Ndanda FC pamoja na wasaidizi wake, Daddy Gilbert ambaye ni kocha mkuu msaidizi pamoja na kocha wa makipa, Willbert Mweta. 

Akizungumza na wanahabari wakati akimtambulisha kocha huyo, Mwenyekiti wa mashindano klabu hiyo, Yusuph Budodi amesema kuwa wameingia makubaliano ya miaka miwili na kocha huyo, pamoja na kipengele cha kuhakikisha klabu inabakia katika nafasi 10 za juu mwishoni mwa msimu huu.

Kwa upande wake, kocha Malale Hamsini baada ya utambulisho amesema, "nimekuja Alliance kwakuwa ni moja ya klabu iliyojipanga na ninajipanga pamoja na wachezaji wangu ili tuiondoe dhana ya kuwa ni timu ya kishule. Timu zote nilizopitia mimi ni za kutumia mpira wa chini, kwahiyo nikiwa hapa Alliance nitauzidisha zaidi ili tucheze mpira wa kuvutia na kupata matokeo".

"Lengo langu katika timu hii ya Alliance ni kuiweka katika viwango vya juu kwakuwa ni timu nzuri, hata nilivyokuja kucheza nao hapa niliwasifia kwa kiwango chao," ameongeza.

Alliance FC inashika nafasi ya 17 katika msimamo wa ligi kuu Tanzania bara,  ikiwa na alama 13 baada ya kucheza michezo 14 mpaka sasa.